CAG abaini kasoro huduma afya ya akili

1 mwezi umepita 184

Matatizo ya afya ya akili.

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini maeneo yenye kuhitaji maboresho zaidi katika utoaji wa huduma bora za afya ya akili nchini na udhibiti wa vifaatiba katika vituo vya afya vya umma.

Ukaguzi umebaini kutokuwapo kwa utambuzi wa watu wenye matatizo ya akili katika ngazi ya jamii na badala yake ulilenga watumiaji wa dawa za kulevya, wazee, watu wenye ulemavu, watoto walio katika mazingira magumu na waliopata mimba za utotoni.

“Hali hii ilichangiwa na ukosefu wa fedha za kutosha kwa ajili ya huduma za ustawi wa jamii na kukosekana kwa maofisa ustawi wa jamii katika ngazi za chini, vikiwamo vijiji na mitaa,” amesema.

Aidha, amesema kuna ukosefu wa huduma za kisaikolojia katika ngazi ya jamii na kubaini kutokuwapo kwa huduma za kisaikolojia ngazi ya jamii, huduma za matunzo ya kisaikolojia na usaidizi kutokuingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti, sera, programu, afua, na mikakati kwa ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za afya.

“Udhaifu huu ulisababisha kutokuwapo kwa huduma kamili kwa makundi mbalimbali, wakiwamo wagonjwa wa akili,” amesema.

Amebaini rasilimali zisizotosheleza (wataalamu, miundombinu, vifaatiba, na dawa) na kutopatikana kwa huduma za utengamo katika vituo vya kutolea huduma hizo ambako kulichangiwa na Wizara ya Afya kutokuwa na mpango wa kuajiri wataalam wa afya ya akili na kutokuwapo muundo wa utumishi unaowajumuisha wahitimu wa taaluma ya huduma za afya ya akili.

Pia, amebaini kulikuwa na ukosefu wa huduma za utengamo kwa ajili ya kuendeleza ujuzi, ushirikiano wa jamii, na misaada inayozingatia urejeshaji, na kwamba kati ya mikoa 28, ni mitano ndiyo ilikuwa na vituo vya utengamo kwa ajili ya huduma za afya ya akili.

Mikoa hiyo ni Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, na Kigoma. 

Aidha, CAG amebaini kuwa kuna udhibiti wa vifaatiba katika vituo vya afya vya umma, na ukaguzi unatambua jitihada za serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzani (TMDA) kwa kuanzisha idara ya kudhibiti vifaatiba.

Ukaguzi umebaini kuwapo kwa vifaatiba visivyofanya kazi katika vituo vya afya vya umma 18 vilivyotembelewa sawa na asilimia 27 ya vifaatiba, huku asilimia kubwa ya visivyo faa vikibainika katika kanda ya kati. 

Kadhalika, umebaini kuwa TMDA haikuwa na kumbukumbu za kutosha ya asilimia 56 ya vifaatiba vilivyosajiliwa, na hakukua na uhuishaji wenye ufanisi wa vyeti vya usajili wa vifaatiba unaofanywa na mamlaka hiyo.

“Asilimia 51ya wenye usajili wa vifaatiba hawakulipa ada ya mwaka ya kuhifadhi. Kutokana na hali hiyo, serikali ilipoteza mapato ya Sh.10,261,473,750 ya ada ya uhuishaji wa usajili wa vyeti vya vifaatiba na kiasi cha Sh. 241,040,000 kwa ajili ya ada ya mwaka ya kuhifadhi vifaatiba vyao vilivyosajiliwa kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2022/2023,” amesema.

Amebaini ni matokeo ya kutokuwa na ufanisi wa udhibiti wa vifaatiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi na vituo vya afya vya umma pamoja na ufuatiliaji na usimamizi duni wa Wizara ya Afya. 

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST