RC Homera apiga marufuku ugawaji viwanja bila idhini

1 mwezi umepita 175

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.

SIKU moja baada ya kutokea maporomoko ya tope lililofunika nyumba 20 na shule moja katika Kata ya Itezi jijini Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amepiga marufuku maofisa ardhi kupima viwanja katika eneo lolote kabla Kamati ya Mipango Miji haijaidhinisha.

Aidha, amepiga marufuku upimaji wa viwanja kwenye maeneo yote hatarishi yakiwamo ya pembezoni mwa mito ambayo inaweza kufurika na kusababisha madhara kwa binadamu.

Homera ametangaza marufuku hiyo alipotembelea eneo lililoathirika na maporomoko hayo ambayo yalisababishwa na kumeguka kwa Mlima Kawetere kutokana na mvua ya masika inayoendelea kunyesha jijini humo.

Amesema nyumba zilizoathiriwa na tope hilo zina hatimiliki zilitolewa na jiji hilo na kwamba endapo kamati ya mipangomiji ingekagua eneo hilo kabla ya kuanza kumilikisha watu kuna uwezekano ingezuia madhara hayo.

“Maeneo yote hatarishi ni marufuku kupima viwanja kuanzia sasa, ni lazima kamati ya mipango miji ijiridhishe kwanza kuhusu usalama wa eneo husika ndipo upimaji uendelee,” amesema Homera.

Hata hivyo, viongozi wa mila wameiomba serikali kuwasikiliza wanapotoa maoni yao kuhusu maeneo yanayopimwa kwa ajili ya makazi wakidai kuwa baadhi ya maeneo yana historia ambazo sio za kawaida.

Katibu wa machifu wa Jiji la Mbeya, Michael Ilanga, amesema eneo hilo maporomoko yalianzia miaka ya nyuma paliwahi kuwapo ziwa dogo ambalo baadaye lilipotea na miaka ya karibuni limerejea tena likiwa na umbo dogo.

Amesema pia kuna mambo ya kimila yalikuwa yanafanywa na moja ya familia kutokana na ndugu yao kupotelea kwenye ziwa hilo miaka ya nyuma kwa kuzama.

Hata hivyo, amesema chanzo cha mlima huo kumeguka ni kukatwa kwa miti iliyokuwa imepandwa na kuruhusu shughuli mbalimbali za kibinadamu, ikiwamo kilimo na ujenzi wa makazi kwenye maeneo hayo ya miinuko.

“Hapa zamani palikuwa na miti ambayo ilipandwa na jiji, lakini walikata miti hiyo na wakapima viwanja, sasa tumekuwa tukitoa maoni yetu, lakini yanapuuzwa, hata pale Mwansekwa viwanja vimepimwa milimani,” amesema Chifu Ilanga na kuongeza.

“Hili eneo pia kuna nyoka na wanyama wengine wadogo, nawaomba wananchi mkimuona huyo nyoka wala kinyonga msiwapige acheni wataondoka wenyewe, tunajua sisi namna tutakavyowaondoa,” ameongeza chifu.

Baadhi ya viongozi wa dini walishauri kwenye maeneo ya miinuko kusifanyike shughuli zozote za kibinadamu, ikiwamo kilimo na ujenzi wa makazi ili kuepuka majanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ayas Njalabaha, amesema kwenye vitabu vitakatifu milima imetajwa kuwa nguzo ya kuzuia udongo kuporomoka na hivyo kitendo cha wananchi kuharibu mazingira kwenye maeneo hayo ndiyo chanzo cha maporomoko.

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST