TANROAD yaagizwa kurudisha mawasiliano barabara zilizoharibiwa

1 mwezi umepita 178

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo kufanya tathmini ya maeneo yote yaliyoharibiwa na mvua ya El-Nino, kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanakuwapo wakati wote.

Ametoa agizo hilo jana bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile aliyehoji kuhusu mkakati wa muda mfupi wa serikali katika kukarabati Barabara ya Gomvu– Kimbiji – Pembamnazi.

Akijibu swali hilo, Bashungwa amemwagiza meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam kufika katika barabara hiyo na kufanya tathmini ya maeneo yote yaliyoribika, ili mawasiliano ya barabara yaendelee kuwapo wakati wote.

Bashungwa amesema Barabara ya Gomvu – Kimbiji – Pembamnazi ni sehemu ya Barabara ya Mjimwema – Kimbiji - Pembamnazi (km 49) ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.  

“Kwa sehemu ya Cheka – Avic (km 2) tayari ujenzi umekamilika, kwa sehemu ya Avic – Kimbiji (km 10) taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi zinaendelea," amesema Bashungwa.

Aidha, amesema ujenzi kwa sehemu iliyobaki ya Kimbiji hadi Pembamnazi itajengwa kulinganana upatikanaji wa fedha.

Kuhusu utekelezaji wa Barabara ya Kibada – Mwasonga (km 41), Waziri Bashungwa amemwagiza mkandarasi kuanza kufanya maandalizi ya ujenzi katika eneo la mradi wakati akiandaliwa taratibu za malipo ya awali.

Kadhalika, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wizara ya Ujenzi fedha za dharura, ili kusaidia kufanyika ukarabati katika maeneo ambayo mawasiliano ya barabara yamekatika kutokana na mvua inayoendelea kunyesha nchini.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Samia ameipa kipaumbele Wizara ya Ujenzi kwa kutoa fedha nyingi zilizoelekezwa katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na ukarabati

Source : Kimataifa

SHARE THIS POST